Wanaochunguza njia, vigezo vinavyotumika kumpata Askofu ni 'wazushi' - Mayala

Na Getrude Madembwe, Geita

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza Mhashamu Anthony Mayala amewataka watu kutosumbua akiri zao kuchunguza njia vigezo vinavyo tumika kupata Askofu na akawaita wale wote wanaofanya hivyo kuwa ni wazushi.

Mhashamu Mayala aliyasema hayo wakati wa kukabidhi funguo za kanisa kwa Askofu Mteule wa Jimbo Katoliki la Geita ,Askofu Damian Dallu,siku moja kabla ya kusimikwa kwake.

Alisema anapopatikana Askofu ni vyema wamshukuru MUngu na wala siyo kuanza kuchunguza Askofu huyu kapatikana vipi.

"Njia za Mungu hazichunguzwi kwani maongozi yake ni ya ajabu, hivyo basi haifai kuchunguza ni jinsi gani Askofu kapatikana na wale wanaojaribu kuchunguza ni wazushi", alisema askofu Mayala.

Alisema hata Mtume Paulo anatukataza kufanya hivyo na badala yake aliwataka waumini hao kuepuka migongano isiyo ya lazima katika kazi zao za kila siku wamheshimu Mungu na wasijigawe katika kufanya kazi zao.

Wakati huo huo; Waamini wa Kanisa Katoliki na Madhehebu mengine wametakiwa wasiwe na imani ya kitapeli bali wawe na imani iliyo komaa.

Hayo yalisemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita,Mhashamu Damian Dallu wakati alipokuwa akifunga seherehe za kusimikwa kwake kuwa Askofu zilizofanyika jimboni humo Jumapili iliyopita.

Alisema ili mtu afanye kazi ya Mwenyezi Mungu,anatakiwa awe na imani thabiti mbele za Bwana.

"Ndugu zangu waamini wa jimbo hili la Geita na waamini wengine ,tunahitaji tuwe na imani ambayo ni hai na tukomae katika Imani hiyo na wala tusiwe matapeli wa Imani" alisema Mhashamu Dallu.Mbali na hilo suala la imani,Askofu Dallu pia aliwataka Mapadre,Walei, Watawa jimboni humo kushirikiana kwa pamoja kwani ushirikiano ndio msingi mzuri katika kufanya kazi ya Bwana.

Aliwataka waamini wa Geita kufanya kazi zao kwa kujiamini bila kutemea msaada kutoka mahali pengine.Askofu alisisitiza kauli yake kwa kunukuu maneno ya aliyekuwa Msimazi wa Jimbo hilo,Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki la Shinyanga,yasema "Bure amekufa, msaada yupo mahututi ila aliyebaki ni kujitegemea".

"Hivyo basi ndugu zangu kwa kutumia mfano huo wa Baba Askofu Balina, naomba tufanye kazi zetu kwa msaada wa Mungu na wetu sisi wenyewe na kamwe tusisubiri msaada kutoka sehemu nyingine" alisema Askofu Dallu.

Mei 6 mwaka huu,Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani,Papa Yohane Paulo wa Pili ,alimteuwa Askofu Damian Dallu (44) kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita.

Julai 30 mwaka huu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alimwekea Wakfu na kumsimika Askofu huyo.

Hadi anateuliwa kuwa Askofu,Mhashamu Dallu alikuwa ni Padre na Mwalimu wa taaluma na Maadili katika Seminari Kuu ya Segerea iliyopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam

Sherehe za kusimikwa kwake zilihudhuliwa na watu mbalimbali akiwemo Rais wa Tanzania,Benjamini Mkapa,Balozi wa Vativan nchini,Askofu Mkuu Luigi Pezzuto na Maaskofu kutoka majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki nchini na viongozi wa madhehebu mbalimbali tofauti na Katoliki.

Paroko auza pikipiki kuchangia Kanisa

lSeminari ya Makoko yapata Gombera mpya

Na Josephs Sabinus, Musoma

PAROKO wa Parokia ya Rwamlimi Jimbo Katoliki la Musoma ,Padre Andrew Zajac,amelazimika kuuza pikipiki yake kwa hiari kuchangia ujenzi wa kanisa

la parokia hiyo na waamini wamesema kitendo hicho ni mafano wa kuigwa.

Habari zilizopatikana mjini Musoma na kuthibitishwa na naye pamoja na Mwenyekiti wa Parokia,Bw.Raphael Mashauri,zinasema paroko huyo wa kwanza parokiani hapo,tangu mwanzo wa parokia mwaka 1998,aliamua kuuza pikipiki yake (Honda) ili kuchangia juhudi za wafadhili na waamini kupanua kanisa hilo.

Shilingi milioni 28 zimekwisha tumika na mbali na mchango wao wa nguvu kazi uliokoa shilingi milioni 2, waumini pia wamekuwa wakitoa michango ya mahindi, mtama, mihogo na kuwapikia mafundi tangu kuanza kwa shughuli hiyo mwaka jana.

Padre Zajac alisema katika mazungumzo na Kiongozi pamoja na Bwana Mashauri kuwa ongezeko la Waamini limechangiwa na ongezeko la watu katika eneo hilo ndio maana imebidi kupanua kanisa.

Parokia hiyo iliyopo kwenye eneo lenye kubwa ya maji na barabara, mwaka jana ilianza utaratibu wa mzunguko wa PICHA YA FAMILIA TAKATIFU (Yesu, Maria na Yosefu) katika jumuiya zake zote na kwa ibada maalum, picha hiyo hukaa kwa kila kaya kwa siku moja.

Viongozi hao wa parokia walisema kuwa mzunguko wa picha hiyo unawaimarisha waamini kiroho "unajua hata ile picha inasuta nafsi mbaya" alisema Paroko.

Licha ya upanuzi wa kuta, paa na mnara parokia inatarajia kujenga tanki ili kuvuna maji ya mvua yenye ujazo wa lita 90,000 na akawaomba wafadhili wasaidie shughuli hiyo inayodai kugharimu shilingi milioni 5, pamoja na umeme.

Hivi karibuni Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Mhashamu Justin Samba aliwahimiza waamini hao kutumia nguvi zao kujileta maendeleo alipotembelea parokia hiyo.

Ingawa aliusifu ushirikiano wa Waamini, Viongozi hao walishauri baadhi ya waumini wa vigango vya pembezoni mwa parokia hasa Bisumwa na Nyabange kuacha tabia ya kumwita padre kwa ibada ya mazishi kisha kuchanganya mila

Naye Mwandishi Wetu anaripoti kuwa;Seminari ya Mtakatifu Pius X ya Makoko iliyopo katika Jimbo Katoliki la Musoma, imepata Mkuu (gombera) mpya kutoka Jimbo la Geita, Padre Raphael Mfumakule,imefahamika.

Padre Mfumakule ameteuliwa kuwa Mkuu wa seminari hiyo badala ya Padre Thomas Kabika Biringi, aliyemaliza kipindi chake cha uongozi Seminarini hapo.

Padre Bilingi ambaye ameiongoza seminari ya Makoko kwa muda wa miaka minne tangu Julai 1996 - Julai 2000, ataendelea kutoa huduma yake ya kichungaji kama paroko wa Parokia ya Nyarubere iliyoko jimboni Geita na atakuwa Mkurugenzi wa Katekesi jimboni humo.

Katika ibada ya kumsimika Gombera mpya na kumuaga anayemaliza kipindi chake cha uongozi wa seminari hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Mhashamu Justin Samba hivi karibuni, alimshukuru Padre Bilingi kwa kazi nzuri aliyoifanya kuiongoza seminari ya Makoko kwa kipindi cha uongozi wake.

Mbali na kumshukuru Padre Bilingi, Mhashamu Askofu Samba aliwataka walimu, wanafunzi na wafanyakazi wote wa jumuiya ya Seminari ya makoko, wawe na ushirikiano mwema na wamsaidie kwa karibu zaidi gombera huyu mpya ili aizoee na kuimudu kazi mapema, Pd. Raphael Mfumakule.

Wakati walimu wanahuzunika kumuaga mpendwa wao Padre Bilingi ambaye alikuwa Mwanzilishi wa PAI (Personality, Ability, Interest) na FIC (Foresight, Insight, Creativity), wanafunzi wengi walionesha kumsikitikia hasa walipokumbuka sera yake, "mnilishe kama nguruwe, niwatumikie kama Punda".

Katika furaha hizo zilizokuwa na mchanganyiko wa huzuni, Gombera mpya alimuasa Gombera muagwa, "Endelea kubuni FIC na PAI bila kusahau sala".

.... TEC yawatahadharisha wananchi kuwa macho na wagombea

Na Charles Hililla, Geita

RAIS wa Baraza la Maakofu Katoliki Tanzania Askofu Severine NiweMugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge, ameitaka jamii ya watanzania kuwa macho na wagombea wanaotoa vitu mbalimbali kwa watu kusudi wawapigie kura wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Alisema kuwa imekuwa ni mtindo kwa mgombea kununua uongozi kwa kutoa hongo ya pombe na khanga kwa kutoka kwa wananchi.

Akizungumza wakati ibada ya misa takatifu ya kusimikwa kwa Askofu Damian Dallu, Askofu Mpya wa jimbo la Geita,Mhashamu Damian Dallu ,Askofu NiweMugizi alisema kuwa ni muhimu wapiga kura kupigia kura viongozi wanaofaa badala ya kutoa kura zao kwa shinikizo la pombe na khanga walizopewa.

"Usipige kura yako kwa shinikizo la kusema kwamba mgombea fulani alinipa pombe na khanga zake sasa na mimi ngoja nilipe fadhira kwa kumpigi kura"alisema Askofu NiweMugizi.

Alisema kufanya hivyo ni kuuza uhuru wako ambapo matokeo yake ni kuathirika kwa uchumi wa taifa na watu wake kwa sababu viongozi wake hawana sifa na kuongeza kuwa maisha ya binadamu hayawezi kuthaminiwa na kitu chochote kile.

Misa ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Damian Dallu ilihudhuriwa na jumla ya maaskofu 22 kutoka majimbo mbalimbali ya kanisa Katoliki nchini akiwemo Balozi wa Vatican nchini Askofu Mkuu Luigi Pezzuto.

Mbali na viongozi wa Kanisa pia alikuwepo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Benjamin Mkapa ambaye alifuatana na mkewe mama Ana Mkapa na Mkuu wa mkoa wa Mwanza Bw. Stephen Mashishanga ambapo viongozi hao waliwakilisha serikali.

Mhashamu Askofu Damian Dennis Dallu alisimikwa rasmi na kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa pili wa jimbo la Geita Julai 30 mwaka huu na Mwadhama Polycarp Kardanali Pengo. Kusimikwa kwake kuwa Askofu wa jimbo hilo kunafuatia kuwa wazi kwa kiti cha Askofu wa jimbo hili kwa takribani miaka 4 iliyopita.

Uwazi wa kiti cha Askofu wa Jimbo hilo kulitokana na uhamisho wa Askofu Aloysius Balina ambaye ndiye alikuwa muasisi wa jimbo hilo lililoanza miaka 15 iliyopita. Askofu Balina alihamishiwa jimbo la Shinyanga Septemba 1997 na tangu kipindi hicho kiti cha Askofu wa jimbo hilo kilikuwa wazi. Askofu Balina aliendelea kuwa msimamizi wa kitume wa jimbo hilo hadi lilipopata Askofu wake Julai 30 mwaka huu.

VURUGU ZILIZO JITOKEZA CCM WAKATI WA UPIGAJI WA KURA ZA MAONI

CUF yasema ni matokeo ya ununuaji wapiga kura kutoka 'vijiweni'

lYasema ruksa wagombea wake kutumia biblia

Peter Dominic na Neema Dawson

CHAMA cha wananchi (CUF) kimesema kuwa vurugu zilizo jitokeza wakati wa upigaji wa kura za maoni za kuwatafuta wagombea Ubunge CCM,zilitokana na chama hicho kununua wapiga kura kutoka mitaani.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa vijana Taifa wa chama hicho Bw. Shahibu Akwilombe wakati alipokuwa akizungumza na Gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni.

Alisema,CCM inawatafuta watu wa kuwaunga mkono wakati watu hao hawana mvuto kabisa na chama hicho.

"Hawa wanalazimisha wanaotafuta kuungwa mkono na watu wasio na itikadi za chama chao ndiyo maana walichapisha hata kadi za bandia na kupinga matokeo". Alisema na kuongeza kuwa wapiga kura hao walikuwa wakibadilika kwa vile walinunulia na kupandikizwa kwa tamaa.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo hakufafanua kwa undani juu ya hayo madai yake dhidi ya CCM.

Mkurugenzi huyo wa vijana wa Taifa wa CUF aliendelea kutamba kuwa chama chake kitahakikisha kinaisambaratisha CCM, katika kinyanganyiro cha Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu. Bwana Akwilombe aliendelea kusema kuwa ziara zilizofanywa na Mgombea Urais kupitia chama hicho, Profesa Ibrahimu Limbupa zimekiletea mafanikio makubwa chama hicho kwa vile kilifungua matawi yasiyopungua 72 mkoani Mwanza na kwamba hivi karibuni chama hicho kinatarajia kufanya ziara Kanda ya Ziwa na Magharibi Mkoani Kigoma.

Zoezi zima la kupiga kura za maoni lililomaliza lilitawaliwa na vituko vya hapa na pale ambapo baadhi ya wagombea katika majimbo walilalamikia vitendo vya rushwa na kuwepo kwa kadi za bandia na kupandikizwa wapiga kura. Zoezi hilo pia lilimalizika huku baadhi ya wagombea ubunge wakongwe kushindwa kutetea viti katika majimbo yao hali iliyopelekea vyombo vya habari kutupiwa lawama juu ya utoaji wa takwimu za waliokuwa wanaongoza katika kinyanganyiro hicho.

Hata hivyo alipozungumza na waandishi wa habari kati kati ya juma lililopita ofisi ndogo ya makao mkuu ya CCM Lumumba , Katibu Mkuu wa CCM Bw. Philipo Mangula alisema suala la mgombea kuongoza katika kura za maoni hakikuwa kigezo cha kuhalalisha ushindi kwa vile majina ya wote waliogombea yatapelekwa katika vikao vya chama na mshindi atapatikana kulingana na vigezo vya uwezo na uadilifu katika chama.

Wakati huo huo,Waandishi Wetu wanaripoti kuwa;Ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa Wananchi kwamba Chama cha Wananchi(CUF) ni cha Kiislam,viongozi wa chama hicho wametoa ruhusa kwa wagombea nafasi mbalimbali kutumia vifungu vya Biblia vinavyo fanana na vile vya Quran.

Kauli hiyo ilitolewa jijini hivi karibuni na Katibu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari hizi. Katibu huyo alisema kuwa wakati mwingine chama chake hutumia vifungu vya Quran katika mikutano yake na hii siyo kwasababu ya udini bali vifungu hivyo hutumika kwa vile vinaigusa jamii."Mbona utawala wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa akitumia mifano katika vifungu vya biblia ambavyo vinaigusa jamii na wananchi hawakusema kuwa chama cha CCM ni chama cha kidini? Alihoji.

Aliongeza kuwa kwa sasa Mtu au mwanachama yeyote atakayejisikia kutumia vifungu vya biblia anaruhusiwa bila ya matatizo yoyote kwani chama hicho si cha kiislamu bali ni cha watu wa dini zote.

Akizungumzia suala la shughuli za uchaguzi mkuu utako fanyika Oktoba mwaka huu,Bw.Hamad alisema kuwa chama hakita jihusisha suala la uchangiaji gharama zozote zile zinazohusiana na uchaguzi.

Alisemea pesa ambayo wataendelea kuchanga ni ile ya shi.100 kwa mwezi ambayo huchangwa na kila mwanachama kwa ajili ya maendeleo ya chama.

"Ndiyo maana unakuta kuna ziara ya kiongozi yoyote yule wa chama cha CUF na kukawa na shamrashamra nyingi za magari, ngoma, bendi vyote hivyo si gharama ya chama hicho ,ni michango inayotolewa na wanachama wenyewe binafsi ambao ni wakereketwa,hali hiyo imekuwa ikijengeka kwa watu wengi kuwa chama hicho kinatumia fedha yake ya ruzuku kwa ajili ya shughuliza mikutano na sherehe"alisema.

Sambamba na hayo aliongeza kusema kuwa chama hicho kiko macho kuwaona, kuwadaka na kuwachukua viongozi wote wazuri watakaojiengua CCM na kujiunga katika chama chao.

"Kama wataonekana ni wazuri na wanafaa katika Uchaguzi ujao,tuko tayari kuwapa majimbo kugombea ili tupate ushindi kwani hilo ndilo lengo letu muhimu"alisema

Pezzuto kuzindua Radio Ukweli

Na Sr.Gaspala Shirima,Morogoro

Leo Balozi wa Vativan nchini,Askofu Mkuu Luigi Pezzuto,anatarajiwa kutembelea Jimbo Katoliki la Morogoro ambapo pamoja na kufanya mambo mbalimbali jimboni humo,vile vile atazindua kituo cha Radio ya Jimbo hilo,Radio Ukweli.

Habari kutoka jimboni humo,zilizodhibitishwa na Askofu wa Jimbo hilo,Mhashamu Telesphor Mkude,zinasema kuwa Agosti 8 Mwaka huu majira ya alasiri,Mhashamu Pezzuto atatoa Sakramenti ya Daraja ya Upadrisho kwa Shemasi,Gregory Matoanya na Shemasi Moses Damos katika ibada ya misa takatifu itakayofanyika katika Kanisa Kuu la Jimbo hilola Mtakatifu Patrisi.

Mhashamu Pezzuto pia atatembelea parokia na vituo zaidi 14 kati ya parokia 53 zilizopo jimboni humo.

Premji atoa Milioni 1.5 kuchangia shule ya Kanisa Katoliki

lNtagazwa atoa sh. 450,000

Na Dalphina Rubyema, Kigoma

MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Mjini (CCM) Bw. Azim Premji ameahidi kutoa jumla ya shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya kujengea shule ya sekondari ya Newman Kilinga iliyopo chini ya kanisa katoliki Jimbo la Kigoma.

Mbunge huyo alitoa ahadi hiyo wakati wa harambee maalum ya kuchangia shule hiyo iliyopo katika eneo la Kigoma vijijini ambapo wananchi mbalimbali mkoani humo walialikwa kushiriki harambee hiyo iliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Kigoma Club.

Premji aliahidi kutoa shilingi 25,000 kila mwezi kwa kipindi cha miaka mitano

"Mimi na"Mimi naahidi kutoa 25,000 kila mwezi kuanzia hivi sasa kwa kipindi cha miaka mitano" alisema.

Hata hivyo Mbunge huyo alionyesha bayana kwamba ahadi yake itatimizwa kama alivyo ahidi hata kama hatafanikiwa kupata tena kiti chake katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na madiwani.

Mbali na Bw. Premiji, Mbunge wa Kibondo Bw. Elikado Ntagazwa naye aliahidi kutoa shilingi 450,000 kwa ajili ya shule hiyo ambapo alifafanua kuwa shilingi 150,000 ni kwa niaba ya mkewe ambaye ni mwalimu na shilingi 300,000 ni kwa niaba yake mwenyewe.

"Unajua mke wangu ni mwalimu, hivyo anaelewa sana umuhimu wa Elimu, ingawa akuweza kufika hapa lakini kwa vile mimi nipo naomba nimwakilishe, ninaahidi kutoa shilingi 150,000 kwa niaba yake na shilingi 300,000 kwa niaba yangu mimi mwenyewe" alisema Bw Ntagazwa.

Kutokana na ahadi za wabunge hao kulifanya jumla ya fedha iliyoahidiwa kwa siku hiyo ikijumlishwa na ile ya waalikwa wengine kufikia zaidi ya milioni tano amabpo pesa taslimu iliyochangwa kwa siku hiyo ni sh. 365,000.

Akitoa neno la kumkaribisha mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Kogoma Bw. Abubakari Mugumia, Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Mhashamu Paul Ruzoka alisema kuwa shule hiyo ambayo inampango wa kuanzisha chuo kitatoa mafunzo ya Sayansi ya jamii kwa Waalimu alisema kuwa inahitaji kwa karibu ushirikiano wa wananchi. Mkuu wa shula hiyo Bw. Sebastian Zabayanga aliwaambia waalikwa katika harambee hiyo kuwa shule hiyo yenye eneo lipatalo hekari 198 ilianzishwa mwaka 1994 na usajili ulifanyika 1996 ambapo ilisajiliwa kama shule ya sekondari na chuo cha Ualimu.Alisema shule yake mbali na kutumika kama sekondari lakini hata hivyo tangu mwaka 1997 imekuwa ikitumika pia kama kituo cha kuendeleza walimu.

Bwana Zabayanga aliendelea kusema kuwa shule hiyo ambayo ina wanafunzi wa kulala na kutwa inatoa masomo ya Historia, Jiografia na Kiingereza (HGL) kwa upande wa kidato cha tano na sita ambapo ada ni sh. 80,000 kwa wale wa kutwa, na shilingi 160,000 kwa wale wa bweni.

Alifafanua kuwa endapo pesa itapatikana shule ina mpango wa kujenga bweni la wasichana wapato 40 ambapo shilingi milioni 41 zinahitajika, maktaba na samani zake( milioni 2.57), zahanati na vifaa vyake (milioni 50), gari dogo(min bus) (milioni 20) na vifaa vya ofisini(milioni3) ambapo aliongeza kuwa ili vitu vyote hivi vikamilike zinahitajika shilingi milioni 116,500,000.

Mgeni rasmi katika Harambee hiyo Bw. Abubakari Mugumia alisema ofisi yake itato mchango wa hali ya juu katika kuendeleza Elimu mkoani humo ambapo kwa siku hiyo alitoa ahadi ya shilingi 200,000.

Walemavu wawaomba viongozi wa dini wawatoe gizani

Na Neema Dawson

WALEMAVU wa macho na viungo vingine wamewaomba viongozi wa dini nchini kuwapelekea huduma za kiroho katika maeneo mbalimbali wanakoishi walemavu hao badala ya kuwaacha waendelee kubaki gizani.

Hayo yalikuwa ni miongoni mwa matatizo na matakwa yaliyotolewa na walemavu wakati wa mashindano ya kusoma Quran Tukufu yaliyoandaliwa na World Muslim Congress Tanzania kwa kushirikiana na Yemen Community ambayo ni ya kwanza kufanyika Barani Afrika.

"Walemavu tumesahaulika katika huduma nyingi zilizo na umuhimu na manufaa kwetu lakini huduma hizo wanapewa watu ambao si walemavu kwani walemavu tunatakiwa tupewe haki sawa na walio wazima" ni kauli iliyotolewa na mmoja wa walemavu wa macho ambaye hata hivyo alikataa jina lake lisindikwe gazetini.

Mashindano hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Starlight jijini hivi karibuni yaliwahusisha walemavu wa macho na viungo mbalimbali kutoka mikoa kadhaa nchini ambapo jumla ya watu 24 walishiriki na kati yao 18 ni wanaume na sita wanawake.

Walemavu hao walisema kuwa wao wamekuwa wakisahaulika kwa muda mrefu bila kupata msaada wa kiroho hali ambayo wataulizwa na Mungu endapo watakufa bila dini na kuongeza kusema kuwa endapo wataulizwa swali ama hilo watajibu"viongozi wa dini waliwaficha gizani bila kuwapa msaada".

Katika mashindano hayo ambayo mgeni rsmi alikuwa ni Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassani Mwinyi,mshindi wa kwanza na wapili walipewa zawafi ya Radio kaseti na tiketi ya kwenda na kurudi Macca kwa ajili ya kufanya hija ndogo

Naye Mkurugenzi Mkuu wa World Muslim Congress Sheikh Mohamed Lukara aliwataka walemavu wa viungo wanaoona kujitokeza ili waweze kupata elimu zaidi na ujuzi mbalimbali.

Mbunge wa Ilala kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)alitoa kompyuta moja kwa ajili ya kusaidia walemavu hao ambayo alisema ikae katika ofisi za World Muslem Congress na itumike kuwapatia mafunzo walemavu wote ikiwa ni pamoja na kuwaongezea ujuzi.

Mashindano hayo yalihudhuriwa pia na mabalozi waliopo hapa nchini kutoka nchi za Algeria, Saud Arabia, Palestina na Yemen ambapo Rais Mwinyi aliwataka waislamu kote ulimwenguni kushikamana na dini pamoja na mwenyezi Mungu na kutojihusisha na ugomvi ambao utawagawa.

Viongozi wanao tumia rushwa wamefilisika kimaadili

Na. Reginald Barhe, Bagamoyo

IMEELEZWA kuwa kiongozi yoyote anayetumia rushwa kutafuta ushindi,amefilisika kimaadili.

Hayo yalisemawa hivi karibuni na mkuu wa mapadre wa shirika la Roho Mtakatifu Kanda ya Afrika Mashariki ,Padre Gerard Nnamunga katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi.

Katika mahojiano hayo yaliyofanyika katika Parokia ya Bagamoyo Jimbo Katoliki na Bagamoyo,Padre Nnamunga alisema watu wa namna hiyo badala ya kutoa rushwa wanapaswa wajiulize nini kwanza wamelifanyia taifa na wala siyo siyo taifa limewafanyia nini.

"Kama alivyosema Baba wa Taifa,Mwalimu Julius Nyerere kwamba kiongozi unayetaka kura za wananchi ni lazima ujiulize nini umelifanyia taifa lako na si taifa limekufanyia nini?"Alihoji.

Wakati huo huo, Padre Nnamungu ametoa rai kwa viongozi wa dini kuwa wawajibike kwa uaminifu katika majukumu waliyokabidhiwa na uongozi wa juu wa kanisa, kwa a manufaa ya jamii.

Alitoa kauli hiyo kufuatia swali la Mwadhishi wa habari hizi kuhusu nini mang’amuzi ya safari ya hija ya kilomita 221 kati ya Mhonda na Bagamoyo inayokamilika jumamosi hii.

Padre Nnamunga alisema amesikitishwa na habari kutoka maeneo kadhaa ambayo waamini wake na wananchi kwa ujumla wake kwamba viongozi wa dini hawajseshi kuestembeles tskribani miaka 17.

Amesema wajibu wa kiongozi wa dini ni kumsaidia mwananchi kwa maendeleo ya ya kiroho na pia maendeleo ya kijamii kama vile maji, afya na shule.

Kiongozi alisema yeye na kundi lake wanafanya hija ngumu kuenzi kazi iliyofanywa na mapadre wa kwanza wa Bagamoyo na Afrika ya Mashariki ambao wengi walijitolea hata kufa wakiwa vijana wasiozidi miaka 25 wakifundisha imani, maendeleo hususan kukomesha biashara haramu ya utumwa wakishirikiana na serikali ya wakati huo.

"Utafundishaje imani kwa mtu aliye na njaa, mgonjwa hana maji wala elimu ya uraia"alihoji.

Wafanyabiashara wa vyakula vya mifugo watakiwa kufuata viwango

Na Gerald Kamia, DSJ

ILI kupata soko zuri katika biashara huria,watengenezaji wa vyakula vya mifugo nchini hususan kuku, wametakiwa kuzalisha bidha zao zikiwa na viwango bora na taratibu za utengenezaji wake na watakao enda kinyume watafungiwa biashara zao.

Akifungua warsha siku moja ya vyakula vya mifugo iliyofanyika katika ukumbi wa kituo cha msimbazi mwishoni hivi karibuni ,Mwenyekiti wa warsha hiyo Bw.A.Boki alisema kuwa "Viwango vilivyowekwa na Tanzania Bereau of standard (TBS) havifuatwi na hakuna mamlaka inayofuatilia" alisema Boki.

Alisema kuwa T.B.S imeweka viwango vyakula vilivyo changanywa kama vile Broiler feedstaffs chicken feed stuffs na ambavyo havijachanganywa kama Blod meal fish meal bone meal.

Bw. Boki ambaye alifungua warsha hiyo badala ya mgeni rasmi Mkurugenzi Idara ya Kilimo (DLD) alisema kutokana na matatizo yaliyojitokeza ,sekta hiyo ya vyakula vya mifugo haiwezi kuendelea vizuri na kuleta ushindani muafaka.

Hata hivyo alisema kuwa inakisiwa kuwa hapa nchini viwanda vipatavyo 72 ambavyo hutengeneza vyakula vya mifugo (hasa kuku) huzalisha tani 320,000 wakati huo huo mahitaji ya vyakula hivyo ni tani 420,000.

Alisema bado kuna pengo la tani 100,000 ambalo lina takiwa lizibwe na watu wanaoshughulika na biashara hiyo.

"Wazalishaji wa vyakula vya kuku wamekuwa hawana umoja ambao utaongeza mshikamano katika kutatua matatizo yao kwa ujumla na hii imesababisha serikali hasa wizara ya kilimo na ushirika, kushindwa kuwasiliana nao vizuri ili kupata ufumbuzi wa baadhi ya matatizo"alisema.

Bwana Boki ameitaka serikali kushirikiana na washika dau kurekebisha sheria ambazo ni za zamani na zimepitwa na wakati na kuwataka wapange uthibiti huo utafanywaje.

Watoto kupelekwa nje ya nchi kusoma

Kunachangia wimbi la vitendo viovu-Pengo

Na Getrude Madembwe, Sengerema

IMEELEZWA kuwa watoto ambao hupelekwa na wazazi wao nje ya nchi kwaajili ya kupata elimu baadhi yao ,husahau kilicho wapeleka huko na badala yake hujiingiza katika vitendo viovu vikiwemo vya utumiaji wa madawa ya kulevya.

"JAMANI madhambi na maovu tuliyonavyo yanatutosha kuyashughulikia na tusijiongezee madhambi mengine".

Hayo yalisemwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam ,Muadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati msafara wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchiniulipotembelea Shule ya Msingi ya Mtakatifu Carol iliyomo katika Jimbo Katoliki la Geita.

Muadhama Pengo alisema watoto wengi wanaenda nje ya nchi kusoma huenda huko wakiwa na adabu nzuri lakini wakisha fika huko hujifunza mambo maovu kwa kufuata pengine mkumbo.

"Sisi wenyewe tunaweza tukawa na shule nyingi za Medium na hata tunaweza tukazungumza Kiingereza kizuri hata kushinda wao". Alisema Muadhama Pengo na kuongeza ‘Wakoloni waliokaa nchini Uganda na Kenya ndio hao waliokaa hapa Tanzania hivyo basi tujenge shule nzuri kama hii ili watoto wetu wabakie hapa hapa na tusiwapeleke nje’.

Akiongea na Mwandishi wa habari hizi shuleni hapo Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bw. John Chamiku alisema kuwa kwa sasa wapo wanafunzi 437 na wana mikondo 10 vyumba 10 vya madarasa na walimu 20.

Alisema kwa sasa wanatumia majengo ya chekechea wakati ujenzi wa shule hiyo ambao unaendelea na wafadhili na kutoka Uholanzi.

Alisema hadi ujenzi huo ukamilike utagharimu jumla ya shilingi milioni 500.

Wakati huo huo: Muadhama Kardinali Pengo amewataka wanafunzi waSeminari Katoliki ya Sengerema kuhakikishe wanashinda tena mtihani wao wa Taifa wa kidato cha nne kama ilivyokuwa mwaka jana ambapo Seminari hiyo ilishika nafasi ya kwanza kitaifa.Alisema kuwa litakuwa ni jambo la aibu kama wao watakuwa watu wa 80 au namba nyingine tofauti na zile za tatu bora."Itakuwa ni jambo la aibu iwapo mtakuwa wa 80 au namba nyingine, lakini mkiwa wa 3 au 2 sio mbaya" alisema Mwadhama na kuwatania kuwa ‘kama mkishika nafasi hiyo ya kwanza Seminari yangu ya Visiga itashika namba ipi muiache nayo iongoze".Aidha Kardinali Pengo aliwataka kuwachanganya wanafunzi wingine yaani watoke Dar-Es-Salaam na sehemu nyingine na sio wawe wa kutoka Shinyanga, Geita, Mwanza na Musoma.

Kigoma wafaidi misaada ya wakimbizi

Na Dalphina Rubyema, Kigoma

PAMOJA na wakimbizi kutoka nchi jirani za Kongo na Burundi kuleta madhara mbalimbali nchini ,wakazi wa Mkoa wa Kigoma wamenufaika na wakimbizi hao ambao huwauzia bidhaa mbalimbali kwa bei nafuuu.

Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa wakimbizi hao wanapoingia kambini hujiandikisha zaidi ya mara moja kwa kubadilisha majina hali inayowafanya wapate vitu vingi vya misaada na kuviuza kwa wananchi.

Bidhaa ambazo zinauzwa na wakimbizi hao ni masufuria na maturubai ambayo hupewa kwa ajili ya kutengenezea mahema ya kujihifadhi. Masufuria hayo hununuliwa na wafanyabiashara wadogowadogo kwa shilingi 1,000- 1,500 ambapo wafanyabishara hao huyauza kati ya sh. 2000 - 4500 na maturubai yenye nembo ya Shirika la Kimataifa la Kuhudumia wakimbizi (UNHCR) huuzwa kati ya shilingi 11,000 - 25,000).

Wafanyabiashara hao maarufu kwa jina la machinga hufanyia biashara yao zaidi katika vituo vya gari moshi.

Hata hivyo mwandishi wa habari hizi alipokwenda kuulizia suala hili kwenye moja ya vituo vya kupokelea wakimbizi kinachoitwa Kibilizi, mmoja wa wahudumu katika kituo hicho alikiri kuwa ni kweli siku za nyuma wakimbizi walikuwa wakijiandikisha zaidi ya mara moja hiyo kujipatia vitu vya ziada vya kuweza kuuza.

Alisema baada ya ujanja huo kubainika hivi sasa kila mkimbizi anayeingia nchini kupitia katika kituo hicho anawekwa muhuri na muhuri huo unadumu zaidi ya miezi sita.

"Hata kama mhusika ataufuta, ni kwamba tuna tochi zetu maalum ambazo tunawamulika na kugundua muhuri huo" alisema muhudumu huyo ambaye alitakataa jina lake lisiandikwe gazetini kwa vile si msemaji.

Aliongeza "Siku za nyuma walikuwa wanatuchezea sana akiri kwani mtu aliweza kujiandikisha hata mara kumi,walikuwa wakibadilisha maji,leo ana jihita Amdani keshokutwa Amri na siku nyingine Lumata".

Kigoma watakiwa kutatua matatizo yao kwa kutumia rasilimali walizonazo

Na Dalphina Rubyema, Kigoma

WANANCHI wa Mkoa wa Kigoma wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutafuta maendeleo hususani ya elimu kwa kutumia rasilimali walizonazo.

Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa huo Bw. Abubakari Mugumia wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili mkoani humo hivi karibuni.

Bwana Mugumia alisema kuwa mkoa wake una rasilimali nyingi sana lakini tatizo lililopo ni kwamba wakazi wake hawajui namna ya kuzitumia.

Alitoa mfano wa miti ya michikichi ambapo alisema mkoa wake una michikichi ya kutosha lakini cha kushangaza na kusikitisha ni kwamba hakuna viwanda vya kukamua mafuta ya mawese na badala yake wanawake ndio wanaofanya kazi hii kwa kutumia mikono.

‘Tuna miwese mingi lakini hatuna viwanda vya kukamua mafuta ya mawese, wanawake ndio wamekuwa wakitumia mikono yao kukamua mawese na kuuza" alisema .

aliongeza wakazi wa mkoa huo hawana budi kuigia nchi jirani ya Burundi ambayo inakiwanda kikubwa cha kukamua mawese.

Mbali na hilo mkuu huyo wa mkoa wa Kigoma alisema kuwa anasikitishwa sana na hali za maisha ya watu wa mkoa huo japokuwa wanapata pesa nyingi kutoka katika sekta ya uvuvi lakini wanaishi katika maisha ya shida.

"Mwaka 1990-1995 sekta ya uvuvi Kigoma iliingiza bilioni 150 lakini hawa wavuvi vazi lao ni shuka, inasikitisha sana" alisema.

Alisema kuzingatia vizuri utumiaji wa rasilimali hizo mkoa huo utaweza kupigana kikamilifu na suala la Elimu linaloelekea kudumaa.

"Kigezo kinachoonyesha kuwa sisi tuko nyuma kielemu ni kwa vile hatuna shule nyingi, mtoto wa mkoa huu anapomaliza darasa la saba kama alama zake hazikufikia asilimia 70-80 hawezi kuchaguliwa kuendelea na sekondari" alisema.

Aliongeza "Katika mikoa yenye shule nyingi mwanafunzi wa darasa la Saba akipata pass Mark ya asilimia 50-60 kunauwezekano mkubwa wa kuchaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza" alisema.

Sabuni ya "Robarts" haimtakasishi mtu-Mwinjilisti

Na Christina Mbezi, DSJ

IMEELEZWA kuwa mwanadamu asafishiki kwa kuoga na sabuni ya "Robert" ama aina nyingine bali sabuni Pekee ya kumsafisha ni Bwana Yesu Kristu.

Hayo yalisemwa na Mchungaji Siprian Salu wa kikundi cha Huduma ya Uinjilisti nyumba kwa nyumba katika mkutano ulioandaliwa na kikundi hicho uliofanyika hivi karibuni katika eneo la Buguruni Marapa jijini Dar es Salaam.

Alisema " Bwana Yesu akiingia kwako atakuosha kwanza na kukutakasa zaidi na bada ya hapo kila neno utakalolisema litakuwa na neema, busara, amani".

Alisema kuna watu wanaojifanya wanadini lakini matendo yao ni machafu"hii ni kwa sababu kila jema wanalotaka kulitenda halitendiki kwa vile hana roho wa Bwana , akiwa na roho wa Bwna atatenda mema.

Alisema wokovu siyo dini mpya bali ni nguvu ya Mungu inapokuja na kukaa kwa mtu na kumsafisha ." Kama ulikuwa na maneno machafu, nguvu hii itakusafisha ,msiwe na kristo wa kuigiza, kuvaa hirizi na vitu vya shetani, hirizi inafunga njia ya kwenda mbinguni"alisema.

Aliongeza kusema kuwa hata kama mtuasali mara 10 au zidi, lakini ajifikirie kuyaacha mawazo mabaya ambayo yanakwenda kinyume na neno Mungu.

Wauguzi watakiwa kutotumia fani yao kama sehemu ya kujipatia utajiri

lShule kutumia milioni 50 kufanya ukarabati

Getrude Madembwe na Leocardia Moswery

WANAVYUO wa vyuo vya uuguzi nchini wametakiwa kutochukulia fani yao kama sehemu ya kujipatia utajiri.

Hayo yalisemwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam,Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alipotembelea chuo cha Uuguzi kilichopo Sengerema katika Jimbo Katoliki la Geita.

"Siku hizi idara ya Tiba imegeuka kama chombo cha biashara kwa sababu wahusika hawajali utu wa mtu bali wanacho jali ni utajiri ambao unatokana na pesa,kitu ambacho hata Bwana Wetu Yesu Kristo hakufanya hivyo kwani yeye aliponya wagonjwa,aliwatoa mapepo wala hakuwatoza pesa yoyote,iweje sisi tujali pesa kuliko utu"alisema Mwadhama.

Wakati huo huo: SHULE ya Msingi Miburani jijini Dar es Salaam iliyopo katika Manispaa ya Temeke inatarajia kutumia milioni 52 kwa ajili ya ukarabati wa majengo na nyumba za walimu.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi ofisini kwake hivi karibuni ,Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw. Iddy Ally Nyundo alisema kuwa vyumba 22 vya madarasa na nyumba za Walimu vitafanyiwa ukarabati ambapo vyoo vya shule hiyo vitabomolewa na kujengwa upya na kuweka korido.

Alisema kuwa ukarabati huo utakao utagharimiwa na Tume Manispaa ya Temeke utafanywa na Wakandarasi watatu ambao kila mmoja atafanya kazi aliyopangiwa ili kuokoa muda na kufanya haraka.

Bwana Nyundo aliwataja wakandarasi hao kuwa ni MK. Building ambaye atakarabati vyoo, TOLETA International naye atakarabati madarasa ya mbele na mkandarasi WATER Building atakarabati nyumba za walimu.Hata hivyo utafanyika katika shule nyingine za Manispaa hiyo.