Askofu ataka nchi Takatifu ibaki kuwa takatifu

YELUSAMU, Israel

ASKOFU Mkuu wa Yelusalemu, Mhashamu Michael Sabaha, ameyaaambia madhehebu 13 ya ki-Kristo kuwa, hata kama vurugu kubwa bado zinaendelea kati ya Islael na Palestina, nchi takatifu lazima ibaki kuwa mahali pa usalama na wokovu.

Akieleza hayo wakati umwagaji damu ukiendelea huko Mashariki ya Kati mnamo Oktoba 12, mwaka huu, Askofu Mkuuu huyo aliwahimiza Wakristo waliohudhuria ibada katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Stefano lililopo jijjini Yelusalemu kujua kuwa, Neno la Mungu lazima libakie mioyoni mwao, wakisikilizana na kulitafakari hata katika mateso na shida wazipatazo.

Askofu mkuu huyo aliwakumbusha Wakristo hao kuwa, kihistoria, Biblia inaeleza kuwa tangu zamani fitina na umwagaji damu vilikuwapo kama vile ilivyo sasa.

Alisema vivyo hivyo, msamaha na wokovu uliokuwapo zama za kale katika mji huo, ni lazima uwepo hata sasa.

Pneumonia yaua mapadre wawili

UINGEREZA,

Mapadre wawili nchini Uingereza, wamefariki dunia kwa ugonjwa wa Pneumonia walipowasili nchini kwao wakitoka Roma walipokwenda kuhiji.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka jarida moja la habari la kikatoliki huko Roma, zimesema kuwa, kumekuwa na hofu katika maeneo yote ambako walikaa mapadre hao wakati wakiwa kwenye hija huko Roma.

Zinasema mshituko huo umewakumba kufuatia taarifa hiyo na kuwataka kuchukua tahadhari mapema kwa kuhofia kuwepo kwa vimelea zaidi vya ugonjwa huo katika maeneo yao.

Imefahamika kuwa maeneo waliyokaa mapadre hao ni pamoja na chuo na seminarini vituo ambavyo vimesimamiwa na Waingereza jijini Roma.

Gombera Msaidizi wa chuo hicho Padre Nicholous Hardson, amesema kuwa hawatakuwa na amani chuoni hapo hadi wataalamu watakapobaini kuwa eneo lao halina vimelea vya ugonjwa huo hatari wa pneumonia.

Hata hivyo, moja ya tahadhari zilizochukuliwa, ni kuwazuia wanafunzi kutotumia maji ya moto yanayopatika katika mabafu yao.

Moi ataka kila Mkenya awe na simu ya mkononi

NAIROBI, Kenya

RAIS Daniel Toroitich Arap Moi wa Kenya, amezitaka taasisi zinazoshughukia sekta ya mawasiliano, kupunguza gharama za simu za mkononi ili kumuwezesha kila mwananchi wa kenya kuzinunua simu hizo.

Moi alisema kuwa, serikali yake itafikiria maombi ya kampuni hizo za simu za mkononi ya kutaka kupunguziwa ushuru na vifaa vingine.

Alisema wakati wananchi wengi wanalalamikia gharama za simu hizo, gharama hizo zinapaswa kupunguzwa ili yafikie kiwango ambacho kila Mkenya ataweza kukimudu.

Moi alisema kuwa, kwa kufanya hivyo, wananchi wa Kenya watapata unafuu katika mawasiliano na kuwa jamii kubwa sasa itaweza kuwasiliana haraka kwa njia hiyo.

Wakati huo huo:Habari kutoka Capetown nchini Afrika Kusini zinasema kuwa, ofisi zote zinazomilikiwa na vyama vya siasa huko nchini humo katika mkoa wa Western-Cape, zimewekwa katika hali ya tahadhari baada ya mlipuko kutokea nje ya ofisi ya chama cha upinzani cha DEMOCRATIC mwishoni mwa juma huko Capetown.

Watu 4 walijeruhiwa na gari moja kuharibiwa vibaya baada ya kulipuka bomu lililowekwa sehemu ya ndani katika gari hilo.

Bomu hilo limekuwa la 11 kulipuka mjini Capetown katika kipindi cha mwaka huu wa 2000.

Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo amesema kuwa ameshauri ulinzi uimarishwe katika mkoa huo.

Jubilei ya watoa damu yaadhimishwa Jumamosi

VATICAN

JUBILEI ya watoa damu kwa wagonjwa duniani inatarajiwa kuadhimishwa Jumamosi hii (Oktoba 21)

Taarifa kutoka kwa Kamati Kuu ya Maandalizi ya Mwaka wa Jubilei jijini Vatican, imesema kuwa kitendo cha kujikana pasipo malipo yoyote katika utoaji damu, kinalinganishwa kabisa na sadaka ya Yesu Kristo mwenyewe pamoja na dhamira yenyewe ya Jubilei Kuu ya Mwaka 2000 inayoahidi upendo na moyo wa kujitolea.

Tukio hili la jubilei limepewa msukumo zaidi na linayashirikisha mashirika mengine ya misaada hiyo likiweamo Shirika la Msalaba Mwekundu.

Taarifa hiyo imesema kuwa jubilei hiyo ya wanaojitolea damu inaanza saa mbili na nusu asubuhi kwa maandamano ambayo yataisha saa nne asubuhi.

Taarifa imesema maadhimisho ya Misa Takatifu yataanza katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro yakiongozwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili.

Wakati huo huo; Oktoba 22, mwaka huu, itakuwa Jumapili ya Wamisionari iliyotanguliwa na Mkutano Mkuu wa Wamisionari kuanzia Oktoba 18 hdi 21, mwaka huu.

Mkutano huo ulitarajiwa kuhudhuriwa na washiriki 1300 kutoka nchi mbalimbali walijorodhesha kushiriki.Hakuna habari zaidi tulizopata kutoka na mkutanao huo lakini habari za awali zilisema,

Wamisionari katika mkutano wao walitarajiwa kutilia maanani mada isemayo YESU ASLI YA UHAI WA WOTE.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kipapa inayoshughulikia uimarishaji wa imani, amesema linapozungumziwa suala la misioni, watu hudhani ni wahusika maalumu lakini mkutano wa kimisionari utakuwa juu ya kufanya kazi za kimisionari, kumtangaza Kristo na kuangalia na kuthibitisha uwepo wa Kristo katika tamaduni tafauti.

Pamoja na yote hayo Katibu Mkuu huyo alizungumzia hali ya umaskini ulimwenguni.